Chama cha ACT- Wazalendo kimepanga kuwasha moto mjadala wa Katiba mpya katika mkutano wake kidemokrasia kilioitisha jijini Dar es Salaam Oktoba 8.
Mkutano huo
unalenga kufufua mchakato wa Katiba Mpya kwa kuzingatia michakato ya
katiba za nchi nyingine za Afrika, alisema Katibu wa itikadi na uenezi
wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alipozungumza na waandishi jijini Dar es Salaam
jana.
Alisema katika kupata uzoefu, ACT Wazalendo imemualika Adabu
Namwamba, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Labour cha Kenya
kilichofanikiwa kubadilisha katiba yake baada ya mchakato mrefu.
Aliwataja wageni wengine kuwa ni mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba
Tanzania, Deus Kibamba ambaye naye atatoa mada kuhusu suala hilo.
Mchakato wa kuandika Katiba mpya nchini umekwama katika hatua ya kupiga
Kura ya Maoni baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushindwa
kukamilisha uandikishaji wapigakura kwa muda uliotakiwa.
Mchakato huo
uligubikwa na vikwazo kadhaa, ikiwa ni pamoja na vyama vinne vya
upinzani na baadhi ya wajumbe kususia kwa maelezo kuwa Bunge liliacha
Rasimu ya Katiba iliyokuwa na maoni ya wananchi na kuingiza sera za CCM.
Katika mkutano huo, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe atawasilisha
mada kuhusu hali ya nchi kwa mtazamo wa chama hicho.
“Kiongozi wetu
atawasilisha uchambuzi mpana wa kina zaidi kuhusu hali ya nchi yetu
kiuchumi, kisiasa na kijamii tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia
madarakani,” alisema.
Pia, mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira,
ambaye aligombea urais mwaka jana, ataeleza uzoefu wake katika uchaguzi,
wakati mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo atachambua
mwelekeo wa chama hadi mwaka 2020.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment