June 11, 2017



MKATABA wa kipa wa Azam FC, Aishi Salum Manula kusaini Simba umevuja kwenye mitandao ya kijamii na unaonyesha mlinda mlango huyo amesaini kwa dau la Sh. Milioni 50 kwa miaka miwili na atakuwa analipwa Milioni 3 kwa mwezi mshahara.
Hata hivyo, mkataba huo unasema, Aishi atalipwa kwa awamu fedha hizo, Sh. Milioni 25 wakati wa kusiani, Milioni 5 kabla ya Agosti 30 na Sh. Milioni 20 atamaliziwa kabla ya Desemba mwaka huu.
Aishi anakuwa mchezaji wa pili tegemeo wa Azam FC kuhamia Simba SC, baada ya aliyekuwa Nahodha wa timu hiyo ya Chamazi, John Raphael Bocco kutangulia pia Msimbazi kwa dau la Sh. Milioni 50 miaka miwili na mshahara wa Sh. Milioni 4 kwa mwezi. Wachezaji wote wanaondoka Azam FC wakati mikataba yao inamalizika mwishoni mwa mwezi huu na mazungumzo ya kusaini mikataba mipya yalishindikana, kutokana na sera mpya za timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake kutotumia fedha nyingi katika kusajili.
Aishi aliyesimama langoni jana katika lango la timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ikilazimishwa sare ya 1-1 na Lesotho katika mchezo wa kwanza wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 aliibukia kwenye timu ya vijana ya Azam FC mwaka 2013.
Na baada ya kupandishwa kikosi cha kwanza chini ya kocha wa wakati huo, Muingereza Stewart Hall haikuchukua muda mrefu kuwa kipa wa kwanza akimpindua Mwadini Ali.
Lakini Azam FC haina wasiwasi juu ya kuondoka kwa Aishi, ikiamini ni fursa nzuri kwa mlinda mlango mwingine chipukizi aliyepandishwa kutoka timu B, Metacha Boniphace Mnata kuanza kuonyesha umahiri wake.

 

Lakini pia, mkongwe Mwadini Ali bado yupo Chamazi na katika ubora wake, huku chipukizi mwingine, Isihaka Kauju anatarajiwa kurejea Julai 10 kutoka Oman alipokwenda kwa majaribio, na wakati huo huo klabu ina mpango wa kusajili kipa mwingine.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE