Watuhumiwa wakifikishwa mahakamani
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania – TAKUKURU, leo
imewafikisha katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es
Salaam, watumishi wawili waaandamizi wa umma kwa tuhuma za kuhusika na
rushwa katika sakata la Escrow.
Watuhumiwa
hao ni pamoja na aliyekuwa Bw. Teophil John, ambaye ni Mhandisi
Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini - REA, anayetuhumiwa
kupokea fedha za Tanzania shilingi milioni 161.4 kutoka kwa
mfanyabiashara Bw. James Rugemarila, fedha zinazodaiwa kuwa zilitolewa
katika mazingira ya rushwa.
Mtuhumiwa mwingine ni Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Rugonzibwa Teophil ambaye kwa mujibu
wa hati ya mashtaka, yeye anatuhumiwa kupokea fedha shilingi milioni
323, kutoka kwa Bw. Rugemarila pia katika mazingira yanayodhaniwa kuwa
ni ya rushwa.
Katika kesi inayomkabili Bw. John, mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Bw.
Leonard Swai amedai mtuhumiwa akiwa kama mtumishi wa umma, alipokea
fedha hizo kupitia akaunti aliyoifungua kwenye benki ya Mkombozi iliyopo
Ilala jijini Dar es Salaam, ambapo Hakimu anayesimamia kesi hiyo, Frank
Moshi, amemwachia mtuhumiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya
dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanye fedha za Tanzania shilingi
milioni 25 kila mmoja.
Aidha, katika shtaka linamkabili Bw. Rugonzibwa, Hakimu Mfawidhi Bw.
Emilius Mchauru amemtaka mtuhumiwa huyo kuwa na mali isiyohamishika
yenye thamani sawa na nusu ya kiasi cha pesa alichokipokea, pamoja na
wadhamini wawili ambao kila mmoja atawasilisha mahakamani hapo fedha za
Tanzania shilingi milioni kumi.
Watuhumiwa wote wametimiza masharti na sasa wapo nje kwa dhamana
ambapo kesi inayomkabili John itatajwa tena Januari 29 mwaka huu wakati
Rugonzibwa ametakiwa afike mahakamani hapo keshokutwa Ijumaa ambapo kesi
yake itatajwa tena pamoja na kupitia kuona iwapo vielelezo vya dhamana
vinakidhi mahitaji ya mahakama.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment