Zaidi
ya wanachama 500 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
wakiwemo viongozi wa kata mbalimbali katika wilaya ya Ludewa mkoani
Njombe, wamekihama chama hicho na kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo.
Wanachama hao wamefikia maamuzi ya kukihama chama hicho huku
wakiwalalamikia viongozi wao wa CHADEMA wilaya na taifa kumkata mgombea
wao wa ubunge jimbo la Ludewa waliyemuhitaji Bwana Okol Haule na
kumuweka mgombea wanayemuhitaji wao bwana Bathoromeo Mkinga.
Mamia ya wanachama hawa kutoka wilaya ya Ludewa, wamefanya maandamano
ya amani kutoka mtaa wa Kilimahewa hadi katika ofisi za chama hicho
zilizopo mjini Ludewa wakiwa na mabango ya aina mbalimbali yakilaani
viongozi wa CHADEMA wilaya na taifa kumkata Okol Haule aliyeshinda
katika kura za maoni kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo hilo.
Hata mara baada ya wanachama hawa kuwasili katika ofisi za CHADEMA
wilaya, viongozi waliingia mitini na kufunga ofisi, lakini dhamira ya
wafuasi hawa wa CHADEMA wakiwemo viongozi wa juu kutoka kata mbalimbali
za wilaya ya Ludewa, haikuishia hapo na wote wakiwa hawana imani tena na
CHADEMA wakaelekea ofisi za ACT Wazalendo mtaa wa Sokoni na kujiunga
nacho.
Huku wakidhamiria kuisambaratisha kabisa CHADEMA wilayani humo,
wanachama hao wakiungana na mgombea wao wanayemuhitaji bwana Okol Haule
wakachoma moto nguo aina ya kombati alizokua akizitumia mgombea huyo,
bendera na kadi za CHADEMA ambapo bwana Haule anasema ameshindwa
kuvumilia ubakaji wa demokrasia uliofanywa na viongozi wa CHADEMA.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment