Nahodha wa zamani
wa Nigeria Daniel Amokachi amejiuzulu wadhifa wake kama meneja wa kilabu
ya ligi kuu ya Nigeria FC IfeanyiUbah baada ya kuhudumu wiki tano
pekee.
Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 42 alikuwa awali
ameeleza hamu yake ya kutaka kushinda vikombe na kuhakikisha kilabu hiyo
inafana.Lakini ameamua kuondoka baada ya msururu wa matokeo mabaya na kutoelewana kati yake na mmiliki wa kilabu hiyo.
“Nasikitika kuondoka baada ya kipindi kifupi hivi lakini kandanda inaendelea,” Amokachi ameambia BBC.
"Nilikuwa shabiki wa kilabu hii kabla ya kuteuliwa kwangu kama meneja kwa sababu ya msingi uliopelekea kuundwa kwake.
"Lakini sasa naitakia kila la heri na nitafuatilia hatua wanazopiga kwa fahari kuu.”
Ripoti zimedokeza kuwa Amokachi hakufurahishwa na sera ya klabu hiyo ya kutumia barabara hatari usiku kurejea nyumbani baada ya kucheza mechi za ugenini.
Msimamo wake ulimfanya kukosana na milionea anayemiliki klabu hiyo, Ifeanyi Ubah.
Mfanyabiashara huyo anaaminika kuchukulia hatua ya kocha huyo kuwa kukaidi mamlaka yake.
Amokachi alikataa kusema lolote alipoulizwa kuhusu suala hilo.
“Soka haitabiriki na hakuna wakati wa kwenda mbele na nyuma,” alisema.
"Imekuwa heshima kubwa kuhusika katika kilabu hii lakini kwa sasa safari yangu imefikia kikomo FC IfeanyiUbah."
0 MAONI YAKO:
Post a Comment