
Hotuba ya Mwenyekiti ACT WAZALENDO katika mkutano wa Mbagala 05/06/2016 :
Kukuza Demokrasia:
Watu wa Temeke,
Vita vya umaskini ni vita vya kutafuta dira na ramani ya mabadiliko. Ndiyo sababu ya kutafuta uongozi, ili kushika nafasi ya kuongoza mikakati ya kutafuta dira na ramani ya kuondoa umasikini.
Mwaka jana tulikuja kwenu kulieleza taifa nia yetu ya kutaka kushika uonogzi wa Nchi yetu kwa ngazi ya ubunge na udiwani. Mlitupokea kwa moyo na nia moja ya kuwasikiliza wagombea wote wakati ule. Leo tumerudi tena kwenu kutumia uwanja huu kuwapa maoni yetu juu ya mambo yanayoendelea nchini na kutoa mapendekezo yetu juu ya suluhu ya baadhi ya mambo.
Sisi raia wa nchi hii kupitia uongozi wa Chama cha Mapinduzi, (CCM) viongozi waliopo na waliopita ndio tumeifikisha nchi yetu hapa ilipo: tangu uhuru hadi leo. Sifa kubwa ya nchi yetu sasa ni umasikini unaosababishwa na sisi wenyewe chini ya mwavuli wa CCM: nchi ya kitu kidogo donge kubwa, nchi ya rushwa, ufisadi, wizi, ujanjaujanja, ulaghai, ubaguzi na upendeleo wa matakwa yetu na hasa rushwa ya kupata viongozi.
Kwa sababu sisi raia na viongozi wetu tumekubali kuachana na misingi ya utu, uadilifu na uzalendo, tumekuwa wasaliti wa maendeleo yetu wenyewe. Tumekataa haki, tumekataa kuwajibika na leo tunafurahia kutumbuana kama wanyama porini. Badala ya kutumbua mafanikio yetu tunatumbua ubaya wetu na tunafurahia kufanya hivyo.
Siku zote nchi yetu itakuwa na viongozi. Kadiri tutakavyojitahidi kuilinda amani ya nchi yetu, tutakuwa na chaguzi za kila wakati, lakini kadiri tutakavyoendesha chaguzi za rushwa, za matumizi yasiyolingana na maisha ya watu wetu, aibu yetu itafuata vivuli vyetu mpaka kaburini. Hatutaweza kujenga demokrasia kwa kuingiza viongozi kwa njia za rushwa.
Rushwa ina tabia moja mbaya ambayo watumiaji wake hushindwa kujipambanua na wasioitumia. Rushwa ina majigambo. Rushwa ina ubabe wa ushindi. Rushwa ina kiburi. Rushwa inapofusha inakupa kufikiri uko juu ya wengine kwa sababu ulifanikiwa kuwashinda kwa bei ya rushwa na si kwa ubora. Rushwa ni mwana mahadaa ana masihara. Rushwa hutendeka gizani na kujidhihirisha mwangani. Rushwa inaaibisha, inaataabisha inazuga, indaganganya. Rushwa ni hatari kwa uhai wa maendeleo ya watu. Weka mbali na wote wenye uhai.!
Serikali ya awamu ya tano imejipambanua kupigana na adui huyu rushwa, tunaiomba ipigane vita hii kwa weledi ujuzi mkubwa na maarifa, kidemokrasia kwa kushirikisha wadau wengine kadiri iwezekananvyo na kwa kuonyesha uongozi wa watu katika eneo hili la utawala. Rushwa na ubadhirifu umelifukarisha taifa. Matumizi mabaya ya mamlaka, ikiwa ni pamoja na urasimu umechelewesha haki za watu kwa ubaguzi na upendeleo.
Mambo haya tumeyazungumza kwa muda mrefu, tumeona hatua zinazochukuliwa na serikali, na sisi raia tuweke mkono wetu,sauti zetu na nia yetu kuongeza nguvu ya kuchukua hatua madhubuti za kuyadhibiti. Napenda kuwapongeza watanzania wote kwa staha na uvumilivu mkubwa ambao tunautoa kwa serikali wakati inajipanga kututumikia kwa weledi, werevu, uadilifu, utu na uzalendo.
Tumekuja hapa kuwashirikisha mambo kadhaa, pamoja na utangulizi huu.
Kwanza kuwashukuru watanzania wote kwa kukitambua, kukikubali na kukipokea chama chetu. Kwa kauli hii nitamke wazi kuwa chama chetu kina mbunge mmoja na madiwani 40. Wakati wa kuomba kura hatukufanikiwa kuwafikia wapiga kura wa majimbo yote licha ya kujitahidi kufika mikoa yote nchini.
Lakini kwa sababu ya kukikubali na kukipokea chama tumefanikiwa kupata madiwani kutoka maeneo mbalimbali na hata maeneo ambayo hatujawahi kufika kabisa kwa majukumu yoyote ya kisiasa. Hii ni imani kubwa sana. Tunawashukuru na tunawaahidi kuwa tutaendelea kulitetea taifa katika uendeshaji wa siasa na hasa katika eneo la kuandaa viongozi makini wa kulitumikia taifa katika maeneo mbalimbali.
Hili ni lengo pana la chama na ni ahadi yangu kama mama Mwenyekiti wa Chama hiki ngazi ya taifa: Jukumu langu kubwa sasa ni kukijenga chama kama chombo cha kupika fikra, kutafuta muafaka wa kitaifa na kuandaa viongozi: kuelekeza vijana wa kike na wa kiume kujitambua, kujikubali, na kujua kuwa hatima ya taifa hili ipo mikononi mwao leo na kesho.
ACT wazalendo kupitia mpango mkakati wetu wa miaka mitano 2016- 2020, tumeweka mikakati ya kuwajengea uwezo vijana wa kike na wa kiume kuhakikisha kuwa wanajifunza uongozi wa umma kiutu, ki-uadilifu, kiweledi na kizalendo. Taifa hili ni mali yenu. Wajibu wetu viongozi ni kuwapa mbinu za kulitumikia. Kwa kauli hii ninawaomba vijana wote wenye mapenzi mema na nchi hii, kujiunga na chama chetu, na kuchota maarifa haya kwa faida yenu wenyewe, kwa faida ya taifa na ulimwengu kwa ujumla.
Wiki hii dunia imempoteza mmoja wa watetezi wa maendeleo ya binadamu na utu, ndugu yetu Mohamedi Ali, bondia wa mchezo wa ngumi. Ali aliwahi kusema hivi: vita vya silaha ni vita vya kubadili ramani, lakini vita vya umaskini ni vita vya kutafuta dira na ramani ya mabadiliko. Chama chetu kimedhamiria kuwa maabara ya kutafuta ramani ya kupambana na umasikini kwa kuandaa viongozi wake kwa waume kushiriki kuitengeneza ramani hii na kuleta mabadiliko ya kweli. Vita vya kupanga ni vita vya fikra, vita vya kujenga na kuimarisha uono wa jamii na kuweka mikakati ya kuifikia ramani hii. Vijana wa Tanzania karibuni ACT sasa, tulishiriki mpango huu wa fikra.
Kama mama kiongozi na Mwenyekiti ninajua kuwa kina mama wenzangu wengi mitaani hawana nafasi nilizowahi kupata mimi. Mwalimu Nyerere aliwahi kuwaasa wanawake waliofanikiwa kupata nafasi kuwasaidia wanawake wengine kufikia hali yao.
Miongoni mwetu kuna wanawake wanaokejeliwa kuwa wategemezi na kuitwa magolikipa, na wanyonyaji. Ninapenda kuwatia moyo wanawake wote wa nchi hii kujitambua kuwa sifa kubwa ya ushindi wa timu za michezo ni golikipa. Timu hazishindi kwa kucheza na kutupiana mpira vizuri. Timu hushinda pale kipa wao akidaka mpira na ama kuisaidia timu yake kushinda ama kuifanya timu shindani ishindwe. Wanawake ni washindi. Tuudake vizuri mpira wa maisha, mpira wa maendeleo, mpira wa uongozi.
Kupitia mpango mkakati wa chama tunampango maalum na ushindi wa wanawake. Mwaka jana katika upya wetu tulifanikiwa kusimamisha wanawake ….kugombea ubunge, wanawake zaidi ya ….kugombea udiwani na tulitoa mgombea urais mwanamke. Hoja yetu si jinsia hasa. Hoja yetu ni kuwa na viongozi walioandaliwa. Chama chetu kupitia mpango mkakakati wake tumeweka mipango maalum ya kuimarisha uwezo wa uongozi wa wanawake na vijana. Ninawaomba wanawake wote wapenda maendeleo ya nchi hii, magolikipa wazuri wajiunge na chama chetu. Tutaimarisha umahiri wenu, tutasadiana kufufua ndoto zenu za kuwa magolikipa mahiri zaidi kwa timu za ushindi. 2020 ninataka wanawake zaidi ya 1000 kushika nafasi za serikali za mitaa, wanwake wengine 3000 kushika udiwani, na wanawake zaidi ya 150 kushika nafasi za majimbo ya ubunge na chini ya rais mwanamke vijana wetu na kina baba watacheza kwa bidii wakiwa na uhakika wa ushindi.
Kwa sababu hii ninawakaribisha wakina mama wapenda maendeleo ya nchi yetu kuungana na chama chetu kuvuna mafao ya kuwa magolikipa mahiri watakaozipa familia zetu na jamii yetu kwa ujumla ushindi dhidi ya umasikini, ushindi wa familia imara zinazoongozwa na kina mama wanaojitambua na kujikubali, na wanaojua kuwa kila goli wanalodaka ni kwa mustakabali wa taifa letu.
Siku ya leo ninawashukuru pia ndugu zetu wa vyama vingine vya siasa ambao wamekubali kushirikiana nasi leo, kusimamia hoja tunayofikiri ilipigiwa kelele na raia wengi juu ya kuruhusu bunge kuendeshwa na matangazo yake kurushwa wazi, kama haki ya msingi ya kupata taarifa sahihi; na watu ama waangalie ama wasikilize popote walipo.
Hoja hii imepata vikwazo vingi bungeni na kijamii, wengine wakiunga mkono na wengine kupinga. Pengine tatizo hasa limekuwa si kuunga ama kukataa lakini jinsi hoja zisizoshibisha akili ya kawaida zinavyotolewa. Kwa kuwa nyuma mambo haya yaliwekwa wazi, kunapotokea mabadiliko ni lazima sababu makini zitolewe, lakini pia kwa sababu ya hali ya kutoaminiana katika mihimili ya uongozi, jambo hili lilihitaji umahiri wa uongozi zaidi kuliko amri na nguvu ya kulazimisha imani. Imani hujengwa. Kazi kubwa ya uongozi ni kutuaminisha kuwa mnaweza si kutulazimisha kuamini mnaweza. Kwa mfano tumeamini kuwa rais magufuli ana dhamira kubwa ya kupambana na matumizi makubwa ya uendeshaji serikali. Tunampa asilimia 100 katika vita hii. Na tunaongeza kusema kuwa vita hii ikiendshwa kidemokrasia, kwa uwazi na wajibikaji, kusikilizana na kuheshimiana inaweza kuleta tija kubwa na kuliokolea taifa mabilioni na matrilioni ya fedha lakini zaidi matrilioni ya imani kwa Rais na ofisi yake. Waingereza wakishukuru kwa furaha husema kimahaba kabisa “ thanks a million!.” Na mimi leo nasema thaks a million Mr president for fighting graft in our public coffers. Asante sana, wajefya ino! Songela zigizigi, waveja, takso mike ndugu Rais. Kwa hatua hii nawe umeingia kundi la wanawake wadakaji wa mipira ya maendeleo. Tunakupa mapenzi yetu yote.
Ugolikipa wa rais katika vita ya rushwa umefanana na wa kina mama. Sawa kabisa. Lakini ukilaza wa wanafunzi hapana, hapana, hapana. Kama mama ninawaomba radhi sana watoto wangu walioingizwa UDOM kwa mpango maalum, wakatolewa kwa mpango maalum tofauti. Hili mheshimiwa Rais hapana! Hili Mheshimiwa Kikwete hapana. Hili waziri Ndalichako, hapana. Mmepotoka,mlipotoka. Mjisahihishe. Mtusaidie na sisi kujisahihisha. Tujifunze utu, uadilifu na uzalendo katika uongozi wa umma.
Aidha ninawakaribisha nyote wawili kujiunga na chama chetu kuimarisha misingi ya uongozi wa umma. CCM inaonekana kuchoka katika eneo hili na ninyi viongozi wema mnaingizwa majaribuni kwa kukosa washauri wazuri katika maeneo haya. Mpango mkakati wetu una wigo mpana wa kujengea uwezo viongozi wa umma kufikia lengo hili. Aidha mama Ndalichako, karibu sana ACT kupata vionjo hivi kuondokana na kauli za kujikinza kila wakati.
Kwa hili niseme kuwa kukinzana kwa kauli zenu juu ya jambo hili imelifedhehesha taifa. Imeshusha hadhi ya ofisi hizi na kushusha imani kubwa ambayo taifa lilianza kujijenga kwenu. Aidha makosa yote ya awamu ya nne yalitakiwa kurekebishwa wakati wa kukabidhiana kazi. Mlikuwa na muda wa kutosha kufanya haya. Kuanikana mbele ya umma kila wakati na kuanza kudhuru raia kama wanafunzi ni kinyume na misingi iliyoasisi taifa letu. Mjisahihishe. Mheshimiwa Kiwete weka wazi mambo yote uliyoharibu wakati wa kipindi chako ujiweke huru. Mafugufuli fanya kazi ya Urais. Waachie wengine majukumu yao, ili sauti yako iwe ya mwisho. Wewe ni size ya super star, be at the top! Remain there. Call us to come there!
Serikali ilipe uzito sana suala la wanafunzi wa UDOM. Tunaomba wanafunzi hawa wasikejeliwe, wasibezwe na haki zao zilindwe. Zisikiukwe. Ujenzi wa demokraisa ya vyama vingi Tanzania itujengee dira ya uongozi wetu. Tujisahihishe.
Katika hili niongeze tena kuwa ujenzi wa demokraisa na vita vya ufisadi vitawezekana tukikamilisha pamoja na mambo mengine mchakato wa katiba mpya. Mheshimiwa ndugu Rais. Maliza kazi hii. Itakusaidia katika mambo mengi mema unayokusudia kwa nchi yetu. Katiba itaimarisha pia utawala wa sheria na Maadili ya viongozi.
Tunahitaji dira ya taifa kwa ujumla. Tunahitaji dira ya taifa ya elimu. Dira hii itokane na maoni ya raia wote kupitia wawakilishi wa wanafunzi,waalimu, wazazi, wanasiasa, wafanyabiashara na mahitaji ya soko la ajira,vyuo nk. Tupate dira ambayo hakuna waziri wala rais ataikiuka.
Tunalikosea taifa, tunawakosea watoto / wanafunzi na waalimu wanaojitoa kwa ajili ya kuelekeza akili zinazokua. Tunatakiwa tujisahihishe jinsi tunavyoendesha nchi, tunavyotoa na kusimamia maamuzi. Yaliyotokea UDOM, na Chuo cha Mtakatifu Joseph ni viashiria vya kukosekana uratibu makini na uongozi katika elimu. Tujisahihishe, tutafute suluhu. Tuanze upya, tuendelee.
Program maalum ni jambo la kawaida katika taasisi za elimu duniani, zisiwe kigezo cha migogoro na zisidhalilishe wanafunzi na waalimu na uongozi wa umma kwa kiasi hiki…tujiahihishe!
Madhila ya kuanzisha shule za kata zilionesha wazi lengo la kutugawa kati ya watoto wa wenye mali na wavuja jasho wa nchi hii…hatutakuwa na maana kukusanya mapato kulipia wenye nacho….na nchi isiyotunza yatima wake ina maana gani huku duniani? Tujisahihishe!
Mauaji ya Kiraia:
Kwa nini mauaji na uchinjaji wa kiraia? Wizara ya mambo ya ndani kulikoni? Kwa nini mnatupa tu taarifa za matukio bila sababu zake na uwezekano wa kupambana na hali hii. Hatujamsikia waziri mwenye dhamana akilipa taifa taarifa sahihi juu ya jambo hili. Nini kinaendelea?
Umma haujasahau mauaji yanayofikirika kuwa ya kisiasa ya ALPHONSE Mawazo, taarifa yake iko wapi, imethibitisha chanzo cha kifo chake? Na tufanye nini kujikinga na aina hiyo ya mauaji? Hatuwezi kuendelea kuishi kwa hofu ya kutokujua vyanzo vya mambo. Hatua gani zimechukuliwa kwa wahusika wa ukatili huu.
Mauaji ya GEITA, ya watu kuchinjwa na miili yao kutenganishwa na vichwa kutokana na imani za kishirikina. Mauaji ya kikatili ya Msikitini mkoani mwanza na kusababisha watu waumini watatu kuuawa. Mauaji ya TANGA katika Kitongoji cha Kibatini yameleta hofu kubwa na hadi sasa hali si shwari maeneo hayo. Wanakijiji wameanza kuhama maeneo hayo kutokana na hofu, kutoweka amani, na wananchi wamekosa utu.
Uadilifu na weledi wa jeshi la polisi na vyombo vingine vya maamuzi ambapo imesababisha wananchi kutojali sheria zilizopo na kujichukulia maamuzi mikononi bila kuogopa na kuheshimiana.
Chama cha ACT wazalendo kinalaani mauaji haya na kuzitaka mamlaka zote za serikali kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto hii inayoaendelea kuitafuna nchi yetu.
Mwisho. Mambo yote mazito yapewe uzito wake. Suala la sukari, elimu bure, na gharama halisi za elimu hata kwa shule binafsi. Mipango ya maendeleo vijijini, ukuzaji wa viwanda, kutengeneza na kuongeza ajira na kuimarisha biashara baada ya kero za bandari na TRA kupunguzwa. Maoni ya wananchi tangu serikali ishughulikie ubadhirifu na rushwa TRA na bandari ni kuwa rushwa imeongezeka na kupata thamani tangu juhudi za awamu hii kushughulikia utendaji wa bandari na TRA.
Ushuru wa kuingiza bidhaa bado ni juu kulingana na bei halisi z bidhaa. Kwa mfano raia aliyeingiza bidhaa yenye thamani ya dolla 100 napotowa ushuru wa dolaa 150, hawezi kutoa heshima kwa TRA kuwa chobo cha umma cha kukusanya mapato halali. Ushuru umeongezeka kupitia mlango wa nyuma. Nyongeza za ushuru hazina risiti na hazitmbuliki. Ndio maana tunasema rushwa imepata thamani.
Serikali iangalie kwa upya jambo hili. Bado kuna malalamiko ya urasimu na utoaji haki mahakamani. Kesi bado zinachukua muda mrefu kukamilishwa. Ucheleweshaji wa kesi hushawishi mazingira ya rushwa na ama kunyim haki za wasiotoa rushwa. Kasi ya mahakama hailingani na kasi na mahitaji ya maendeleo ya sasa.
Maisha yanazidi kuwa magumu wakati serikali haionekani kuja na suluhu ya mambo. Tunaunga mkono mapambano dhidid ya rushwa. Tunapinga dalili za kubinya demokrasia na kuingilia utendaji kazi wa mihimili mingine. Katika mazingira ambayo nchi imejaa rushwa, imani kwa vyombo vya umma inapungua kila kukicha, tunahitaji mbinu mbadala za kupambana na rushwa kwa kuimarisha imani na vyombo vya umma.
Let your graceful words fly out into the World, carried on winds of courage, imagination and joy. Let them inspire others to step into action
0 MAONI YAKO:
Post a Comment