
Imetolewa leo Tarehe -8/9/2016
SERIKALI YA CCM NA RAIS JOHN MAGUFULI WASIACHIWE WAHARIBU UCHUMI WA TAIFA LETU
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi) kimesikitishwa na taarifa zilizolipotiwa na vyombo vya habari juu ya hali na muelekeo wa uchumi iliyotolewa na Naibu waziri wa fedha na mipango Dk. Ashantu Kijaji, akijibu maswali bungeni jana, kwa ujumla kuna tatizo la aina ya uongozi aliokuja nao Rais Magufuli katika kuongoza nchi yetu, ufanywaji wa maamuzi ya kukurupuka na matumizi ya vitisho na nguvu kwa wadau wa maendeleo, wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi. Tatizo hili la Ombwe la uongozi linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka. Taarifa zinaonyesha kuongezeka kwa deni la Taifa , kushuka kwa ukuaji wa uchumi kwa asilimia 4 kutoka asilimia 9.5, kushuka kwa ukuaji wa sekta ya ujenzi, ukuwaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka asilimia 14.50 robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 7.9 ndani ya robo ya kwanza mwaka 2016, deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 18 na kufikia trilioni 51, ukosefu wa ajira rasmi, maisha ya wananchi hasa wenye kipato cha chini yamekuwa magumu zaidi mbali na tawkimu kuonyesha tofauti na uhalisia.
‘Utumbuaji wa majibu’ hauwezi kuwa ni sera ya Taifa, unapaswa kuunganishwa katika utendaji wa shughuli za serikali za kawaida, pale inapotokea tu (by the way). nchi yetu imekosa kuwa na Dira na vipaumbele sahihi vya kujenga misingi imara endelevu ya maendeleo ya kiuchumi, demokrasia na utawala bora umevurugwa kabisa. Hakuna muendelezo wa masuala mazuri yaliyoachwa na awamu zilizopita na badala yake Rais Magufuli anabomoa na kuuvuruga uchumi wa nchi. Hivi serikali kuhamia Dodoma ni kipaumbele cha sasa kama Taifa?, mwananchi wa kawaida ananufaika nini na hili? Mpango huu ulizingatiwa katika bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17 iliyopitishwa hivi karibuni na bunge la bajeti? Ni wazi kuwa hatua za haraka zinahitajika kuchukuliwa kabla ya mambo kuharibika zaidi.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) kinatoa wito kwa watanzania wote bila ya kujali itikadi za vyama vyetu kama Taifa, tuna wajibu wa kushiriki kwa namna tofauti tofauti wakiwemo wasomi, viongozi wa dini, viongozi wastaafu waliotumikia Taifa letu, wabunge wa vyama vyote. Kujitokeza na kutafuta njia za kumshauri Rais Magufuli airejeshe nchi yetu katika misingi ya demokrasia, utawala wa sheria, maendeleo ya uchumi endelevu kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Lengo na madhumuni ya chama cha CUF katika eneo la uchumi limeainishwa vizuri katika katiba yake ibara ya 7(18) inaeleza kuwa;
“ kujenga uchumi wa taifa ulio imara na unojitegemea kwa kiwango kikubwa na kulitoa Taifa la Tanzania kwenye umasikini na ufukara wa kujitakia na badala yake kulielekeza taifa kwenye neema yenye manufaa kwa wote kwa kutekeleza sera zitokanazo na itikadi sahihi ya uliberali”
HAKI SAWA KWA WOTE
____________________________________
SALIM BIMANI
MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA
MAWASILIANO: 0777 414 112 / 0752 325 227
0 MAONI YAKO:
Post a Comment