Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetuma salamu za shukrani kwa
Gavana wa Jimbo la Akwa Ibom, Gabriel Emmanuel kwa zawadi ya dola za
kimarekani 10,000, (sawa na Sh milioni 21.7) kwa timu ya Mpira wa Miguu
ya Tanzania ‘Taifa Stars’, baada ya kuonesha mchezo mzuri na wa
upinzani dhidi ya wenyeji, Timu ya mpira Super Eagles ya Nigeria
uliofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabo, mjini Uyo.
Taifa Stars ilicheza mechi hiyo siku ya
Jumamosi Septemba 3, 2016 katika mchezo wa mwisho wa hatua za makundi
kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON
2017). Katika mchezo huo ambao mashabiki waliingia bure, Taifa Stars
ilifungwa bao 1-0 licha ya kuibana Super Eagles kiasi cha kumfanya
Gavana huyo kuandaa hafla ya chakula cha jioni (Dinner) ambako mbali ya
kuizawadia kiasi hicho Taifa Stars, pia aliizawadia Super Eagles dola za
kimarekani 35,000.
Taifa Stars ilitua Dar es Salaam usiku
wa kuamkia leo Septemba 5, 2016 ambako baadhi ya wachezaji walipelekwa
Hoteli ya Urban Rose, iliyoko katikati ya Jiji la Dar es Salaam wakati
wengine hususani wale wa timu ya Azam FC walichukuliwa na viongozi wao
kwa ajili ya safari ya kwenda Mbeya ambako Jumatano wanatarajiwa kucheza
na Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
utakaofanyika Uwanja wa Sokoine mjini humo.
Wakati nyota hao 18 wakiwa wamerudi Dar
es Salaam, Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta aliishia Nairobi, Kenya
ambako aliunganisha ndege ya kwenda Brussels, Ubelgiji anakocheza mpira.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment