Siku
moja baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
kuwasimanga viongozi wa Ukawa kuhusu namna walivyompokea Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa na kumteua kuwa mgombea urais, viongozi hao jana
walikutana katika kikao kilichotarajiwa kujadili suala hilo.
Kikao
hicho cha Ukawa kimekuja zikiwa zimepita siku nne baada ya Lowassa na
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kukutana nyumbani kwa
Lowassa Jumatatu ya wiki hii.
Juzi,
katika mahojiano na kituo cha redio cha Clouds FM, Profesa Lipumba
alisema mkutano wa chama hicho ulioridhia Lowassa kuingia Ukawa
ulifanyika Zanzibar bila yeye kuambiwa, kitendo kinachoonyesha kuwa
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa akimzunguka.
Mbali
na tuhuma hizo, kiongozi huyo alieleza kuwa hatakuwa tayari kuona CUF
ikinunuliwa kwa bei chee na Lowassa au Chadema hata kama atakuwa nje ya
chama hicho.
Jana
jioni, viongozi wa vyama hivyo walikutana faragha kwenye ofisi za
Lowassa zilizopo Mikocheni. Haikuweza kufahamika mara moja ajenda za
kikao hicho lakini habari kutoka ndani ya vyama hivyo zilisema pamoja na
mambo mengine kilitarajia kujadili shutuma zilizotolewa na Profesa
Lipumba.
Suala
jingine lililotarajiwa kujadiliwa na viongozi hao washirika wa Ukawa ni
mkakati wa pamoja wa namna ya kuendesha shughuli za siasa katika
kipindi ambacho imetolewa amri ya kuzuia maandamano na mikutano ya
siasa.
Baadhi
ya viongozi waliohudhuria kikao hicho ni mwanasiasa mkongwe nchini,
Kingunge Ngombale-Mwiru aliyewasili saa 10.56 jioni, Mwenyekiti wa Ukuta
Profesa Mwesiga Baregu aliyewasili saa 11.06 akafuatiwa na Maalim Seif
saa 11.13, na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe saa 11.18 jioni.
Mbali
na kikao hicho, viongozi mbalimbali wa CUF, walijitokeza kumjibu
Profesa Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti katika kipindi cha mapambano ya
kukiondoa madarakani chama tawala, CCM, lakini kauli ya pamoja ya
viongozi hao ndiyo inasubiriwa kukata mzizi wa fitina.
Juzi,
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Profesa
Lipumba ni “kigeugeu” huku Mbowe akisema “hakutegemea maneno hayo
yangetoka kwa mtu kama Profesa Lipumba.”
Jana
asubuhi akitumia kituo cha Clouds FM, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Mahusiano wa CUF, Mbarara Maharagande alisema siyo kweli
kwamba Profesa Lipumba hakushirikishwa katika ujio wa Lowassa bali yeye
ndiye aliyepeleka taarifa katika Baraza Kuu la chama kwamba Ukawa
wamekubaliana kumsimamisha Lowassa.
“Alichokuwa
anakifanya Maalim Seif ni haki yake kikatiba kushirikiana na viongozi
wengine wa Ukawa. Mbona yeye alikwenda kumfuata Mzee Joseph Warioba
kumshawishi agombee urais?” alihoji.
Maharagande alisema CUF walimtazama Lowassa kama sura ya kuleta mabadiliko kwa yale waliyokuwa wakiyataka katika Ukawa.
“Profesa
Lipumba alimtazama Lowassa kama mtu wa kawaida, lakini CUF walimtazama
kama kiongozi mwenye ushawishi mkubwa kwa sababu ya uwezo wake wa
kuunganisha wanasiasa,” alisema.
Pia,
jana mchana Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema Profesa Lipumba
ambaye ni msomi ameanguka kifikra kutokana na kauli zake na ukweli
uliopo.
Lissu,
ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki alitoa kauli hiyo baada ya
kuulizwa swali na waaandishi wa habari katika mkutano wake jana
waliotaka kujua msimamo wake kutokana na matamshi aliyoyatoa Profesa
Lipumba.
“Kwa
kifupi ya Profesa Lipumba yasiwasumbue CUF na wala Chadema
hayatusumbui. Wanaosumbuka ni wale wanaomtumia Profesa, kwa sababu
ukweli uko wazi kutokana na mambo yaliyojitokeza baada ya ujio wa
Lowassa,” alisema Lissu.
Alisema
katika chaguzi zote ambazo Profesa Lipumba alikuwa akigombea urais, CUF
Bara haikuwahi kupata viti vya ubunge zaidi ya viwili lakini mwaka jana
kimepata viti 10 kutokana na ushirikiano wa Ukawa.
Lissu
aliwahi kumwelezea Lowassa kuwa pamoja na shutuma nyingi anazorushiwa
nchini bado ni tembo katika uwanja wa siasa ambaye “ukifumba macho yupo,
ukisema hayupo, yupo pale.”
Lowassa
kama “jongoo mpenda watu na watu hawampendi” alisababisha zogo kubwa
ndani ya CCM wakati wa mchakato wa kuteua mgombea urais na jina lake
lilipokatwa aliamua kutulia.
Kutokana
na ushawishi mkubwa alionao katika jamii, Chadema walimfuata kumwomba
ajiunge nao na akateuliwa kuwa mgombea urais na baadaye alinadiwa kwa
vyama vinavyounda Ukawa vya CUF, NCCR-Mageuzi chini ya James Mbatia na
NLD chini ya hayati Dk Emmanuel Makaidi.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment