Mwimbaji mkongwe nchini wa muziki wa dansi, Shaban Dede amefariki dunia asubuhi ya leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.
Dede, ni mwanamuziki mkubwa ambaye alikuwa akiitumikia Msondo Music Band lakini huko nyuma aling’ara na Bendi za Mlimani Park “Sikinde”, Bima Lee, alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya sukari pamoja na figo.
Hamad Dede ambaye ni mtoto wa marehemu, ndiye aliyethibitisha kifo cha baba yake asubuhi na kwamba watatoa taarifa baadaye juu ya ratiba ya mazishi.
Kimuziki Dede ambaye alipachikwa jina la Kamchape na mashabiki wake, alikuwa hodari wa kutunga na kuimba nyimbo za maudhui na ujumbe mzuri katika jamii.
Bendi aliyodumu nayo kwa kipindi kirefu katika maisha yake ni Msondo Ngoma, alikuwa kiongozi pamoja na mzee Saidi Mabera ambaye pia ni mpigaji wa gita la solo.
Alikuwa akishirikiana kuimba katika Bendi ya Msondo na waimbaji Juma Katundu, Twaha Mohamed, Hassan Moshi William ‘TX Junior’ na Hussein Kalembo.
Nyimbo alizotunga ni nyingi na alizoimba pia ni nyingi kama vile Kilio Cha Mtu Mzima, Kaza Moyo (Msondo), Diana, Tui la Nazi, Amina (Sikinde), ambazo zinaonesha uhalisia wa maisha ya watu na zilijizolea umaarufu katika kumbi mbali mbali za muziki na kuvuta mashabiki wa rika zote. Sauti zao zilikuwa zikienda sambamba na wakung’utaji magita ya solo na rhythm ambao ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge, Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’ nao hupiga gita la Rhythm.
Kwa upande wa gitaa zito la besi Dede alipokuwa akiimba sauti yake ilipambwa na gitaa zito la besi la akina Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’.
Na kwenye drums alikuwa akichanganyiwa na Saad Ally ‘Mashine’ na Arnold Kang’ombe wakati tarumbeta alikuwa akipuliziwa na kijana machachari Roaman Mng’ande na Hamis Mnyupe huku tumba zikipigwa na Dorice George na Amiri Said Dongo.
Dorice George ni mwanamuziki mpya wa kike mwenye vipaji vingi. Ni tunda la Chuo cha Sanaa Bagamoyo, bado yupo kwenye majaribio. Lakini licha ya wanamuziki hao, Dede aliwahi kufanya kazi na baadhi ya wanamuziki ambao wamekwisha tangulia mbele za Mungu akiwemo Mzee Muhidini Gurumo.
Wengine ni TX Moshi William, Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, Mustafa John Ngosha, Suleimani Mwanyiro, Tino Maselenge ‘Arawa’, Athuman Momba na mpulizaji wa saxophoni Alli Rashidi aliyefariki dunia siku ambayo bendi hiyo ikitimiza miaka 50, Oktoba 10, 2014.
Dede akiwa Msondo, atakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa akiipenda bendi hiyo kwani licha ya kuihama na kwenda kwa wahasimu wao Mlimani Park Ochestra ‘Sikinde’, alirejea Msondo na hakuhama hadi kifo kinamchukua.
Bendi hiyo ya Msondo ilikuwa na vituko vingi leo nikupeni hiki kimoja ambacho nilikishuhudia miaka ya 1980.
Ilikuwa ni pale ni pale Sokoni Kariakoo. Wakati wa kupokea mbio za mwenge. Kuna ofisa aliwaalika Msondo waje kuburudisha. Msondo wakaja na mashabiki wao basi Mwenge ukaja ukatua salama kabisa.
Msondo wakaanza kupiga muziki huku Dede na wenzake wakiimba kwa umahiri mkubwa na mashabiki wakaanza kucheza. Muziki ukawa unazidi kukolea.
Mashabiki nao wakawa wanapagawishwa na sauti ya Dede ndipo shabiki mmoja akauchomoa mwenge kwenye stendi yake akaanza kucheza nao.
Polisi wakamkimbilia kutaka kumnyang’anya. Yule jamaa akaupasia kwa shabiki mwingine. Mara mashabiki wakauzunguka mwenge. Polisi wakaanza kuwapiga virungu.
Mashabiki wakawa wanapigwa virungu lakini mwenge wakawa hawauachii, hali ikazidi kuwa tete, viongozi wa serikali wakaamuru Msondo wazime muziki, ukazimwa.
Baada ya muziki kuzimwa mashabiki wakaanza kufanya fujo zaidi na kuanza kuondoka na Mwenge toka eneo la tukio. Polisi wakazidisha ukali wakafanikiwa kuuokoa mwenge na kuurudisha kwenye stendi yake na kuuwekea ulinzi maalum.
Kutokana na patashika hiyo Msondo hawakupewa tena nafasi ya kupiga, Dede alikuwa mahiri kwa kuimba, lakini hapo akuimba tena na sherehe zikaisha salama baada ya hapo.
Dede alikuwa na tabia ya kuwapiga dogo wahasimu wake Sikinde, katika onesho lao na Sikinde la hivi karibuni katika viwanja vya Leaders Club moja ya nyimbo zao, Dede na Juma Katundu wakawa wanachomekea kionjo kilichowakejeli Sikinde.
Dede alikuwa akiimba hivi: ‘Zanzibar!’ kisha Juma Katundu akajibu ‘Za uso’, wakarudia hivyo mara kadhaa kabla ya Dede kuhitimsha kwa kusema ‘Hawatakwenda tena’ na Juma Katundu akamalizia kwa neno lile lile ‘Za uso’.
Nilipomuuliza marehemu Dede alikuwa na maana gani alisema hilo ni dongo la Sikinde baada ya maonyesho ya ya Zanzibar kwenda vibaya na kupata mahudhurio kiduchu na hivyo kuwa ni sawa na wamepigwa ngumi za uso. “ Zanzibar ni kama ngome yetu hivyo kitendo cha Sikinde kwenda kufanya maonyesho ya mwendelezo wa sherehe za Idd huko Zenji, tulifuatilia maoneshoi yao na kugundua walikuwa za uso,” alisema Dede.
Sauti ye Dede itaendelea kusikika katika nyimbo nyingi alizoimba akiwa Bima Lee, Sikinde na Msondo.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
Na Elvan Stambuli | Global Publishers
0 MAONI YAKO:
Post a Comment