
Mfanyakazi wa hoteli za kitalii za andBeyond Serengeti, Moses Muhina
aliyetajwa kuwa ni miongoni mwa abiria waliofariki dunia katika ajali ya
ndege ya Shirika la Coastal Aviation, imebainika alibadili ndege muda
mfupi kabla ya safari ili kuwahi kazini. Muhina ambaye ni mwongozaji
watalii katika hoteli hiyo, alikuwa aondoke na ndege ya Coastal Aviation
saa nne asubuhi lakini viongozi wa hoteli walimbadilishia ndege, hivyo
aliondoka na Air Exel iliyofika salama Serengeti.

Akizungumza na gazeti hili, meneja uendeshaji wa Hoteli ya andBeyond
Serengeti Under Canvas, Mussa Matala alisema Muhina ambaye anasomeka
kwenye orodha ya ndege kama Maina alikuwa apande ndege hiyo lakini
walimbadilishia. Alisema waliomba aondolewe kwenye orodha ya wasafiri wa
ndege hiyo lakini kwa bahati mbaya hadi ndege ilipoondoka jina lake
lilikuwapo. Wakati huohuo, raia watano wa kigeni ambao walifariki dunia
katika ajali hiyo, akiwamo rubani Dewald Raubenheimer raia wa Afrika
Kusini, ambaye kwenye orodha ya awali ya waliofariki jina lake
halikuwapo anatarajiwa kusafirishwa leo.

Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya
mkoa ya Mount Meru, Francis Costa alisema miili mitatu kati ya 11
imechukuliwa na ndugu zao. Alisema miili iliyochukuliwa ni ya ndugu
wawili waliokuwa wakurugenzi wa Masai Wondering, Nasibu na Shatri
Mfinanga. Mwingine ni wa Joyce Mkama ambaye alikuwa mfanyakazi wa Hoteli
ya Serena. “Uchunguzi wa miili ya wageni kutoka nje ya nchi unaendelea
na ukikamilika itasafirishwa kwa mazishi katika nchi za Afrika Kusini,
Ujerumani na Italia,”
alisema. Ndege hiyo namba 5H-EGG aina ya Cessna Grand Caravan
ilianguka baada ya kugonga kingo za creta ya Empakai, umbali wa mita
3,250 kutoka usawa wa bahari ikitoka Kilimanjaro kwenda Hifadhi ya
Serengeti. Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema
uchunguzi unaendelea kuhusu ajali hiyo.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment