January 14, 2018

Baada ya miaka miwili, hatimaye Sheikh Zakzaky aonekana mbele ya waandishi wa habari 
Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye kwa miaka miwili sasa anashikiliwa kinyume cha sheria, kwa mara ya kwanza jana aliruhusiwa kuzungumza na waandishi wa habari.

Ripoti kutoka Nigeria zinasema kuwa, Sheikh Zakzaky kwa mara ya kwanza jana Jumamosi alionekana hadharani na kuruhusiwa kuzungumza na baadhi ya vyombo vya habari.
Picha zilizoenea zinamuonyesha Sheikh Zakzaky akiwa anazungumza na vyombo vya habari huku akiwa na kifaa cha kitiba  shingoni maarufu kama (Neck supporter).  Kifaa hiki huwekewa mtu aliyejeruhika shingoni. Hata hivyo haijajulikana hasa alikuwa akizungumza kutokea wapi.
Sheikh Ibrahim Zakzaky akizungumza na vyombo vya habari
Wakati huo huo maandamano ya amani yanayoshinikiza kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky yameendelea kufanyika katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. Maandamano hayo jana yaliyofanyika katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja na kushuhudia washiriki wake wakipiga nara za kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky.
Aidha waandamanaji hao wamesisitiza kwamba, Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anashikiliwa kinyume cha sheria na vyombo vya usalama vya nchi hiyo, hivyo anapaswa kuachiliwa huru mara moja. Vyombo vya usalama mjini Abuja vilivamia maandamano hayo ya amani na kuwatia mbaroni wanachama saba wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni na jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 baada ya kuvamia makazi yake katika mji wa Zaria jimboni Kaduna na kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu. Hata hivyo licha ya mahakama kutoa hukumu ya kutaka kuachiwa huru mwanazuoni huyo, bado vyombo vya usalama vya Nigeria vinaendelea kumshikilia katika korokoro isiyojulikana.

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE