
Mhandisi
Mshauri wa Kampuni ya Nicholas O’Dwyer, Frank Lynham, akitoa maelezo
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa,
kuhusu hatua ya maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara yenye
urefu wa KM 66.9 inayojengwa kwa kiwango cha kisasa cha lami, wakati
alipotembelea kambi ya mkandarasi, mkoani Morogoro.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati),
akikagua eneo la Ruaha lililopo katika Wilaya ya Kilombero ambapo ujenzi
wa daraja kubwa lenye urefu wa mita 130 linatarajiwa kujengwa katika
barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9, mkoani Morogoro. Kulia ni Meneja wa
Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro Mhandisi Dorothy Ntenga.
Muonekano
wa daraja la zamani katika eneo la Ruaha ambapo litajengwa daraja kubwa
la Great Ruaha lenye urefu wa mita 130 katika barabara ya Kidatu –
Ifakara yenye urefu wa KM 66.9, mkoani Morogoro.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa KM 66.9 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Morogoro.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na Mkuu wa
Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo, wakisalimia wananchi wa kijiji cha
Sululu, wilayani Kilombero mkoani Morogoro mara baada ya kukagua kambi
ya Mkandarasi anayejenga barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa KM
66.9, kwa kiwango cha lami.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto),
akizungumza jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo (kulia),
katika ziara yake ya kikazi wilayani humo, mkoani Morogoro.
Serikali
imesema imeanza ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa KM
66.9 kwa kiwango cha lami ambapo kukamilika kwake kutachochea maendeleo
ya kiuchumi na kijamii katika wilaya za mkoa wa Morogoro.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa
Makame Mbarawa, alipokuwa akikagua maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo
ambapo amemuagiza mkandarasi wa kampuni ya Reynolds Construction kutoka
Nigeria anayejenga barabara hiyo kujenga kwa viwango na kukamilisha kwa
wakati.
“Mradi
huu umesuburiwa kwa siku nyingi na wananchi wa wilaya hii na mkoa
kiujumla, mategemeo ya Serikali ni kuwa mradi huu utaukamilisha mapema
mwezi Aprili, 2020 kwa kuzingatia vipengele vya mkataba na kwa viwango
stahiki”, amesema Prof. Mbarawa.
Amesema
kuwa ujenzi katika barabara hiyo unatarajiwa kuhusisha ujenzi wa
madaraja makubwa mawili, madaraja madogo manne, makalvati makubwa na
madogo 271 na unatarajiwa kudumu kwa miaka 20.
Aidha,
Prof Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itahakikisha wananchi wa mkoa
huo wanapewa kipaumbele kwenye ajira mara tu kazi itakapoanza ili
kuongeza kipato chao.“Mradi
umeanza na nimemuelekeza mkandarasi kuajiri afisa mwajiri ili
kuhakikisha nafasi nyingi za ajira zinapatikana kwa wazawa kwani nafasi
70 walizoajiri mpaka sasa ni za mwanzo tu, ila nafasi nyingine
zitaongezwa”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Bw. James Ihunyo, ameipongeza
Serikali kwa jitihada inazozifanya kuboresha miundombinu ya barabara
hapa nchini na amemuahidi Waziri Prof. Mbarawa kuwa wananchi na uongozi
wa usalama wa Wilaya yake watatoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili
waweze kunufaika na mradi huo mapema.
Naye
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro, Mhandisi
Dorothy Ntenga, amesema kuwa kazi halisi itaanza mwishoni mwa mwezi
Februari mwaka huu na watahakikisha wanamsimamia mkandarasi kwa karibu
ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na viwango.
Ujenzi
wa barabara ya Kidatu-Ifakara KM 66.9 kwa kiwango cha lami unatarajiwa
kujengwa kwa miezi 30 na utagharimu kiasi cha shilingi
bilioni
111.4 na unafadhiliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (European Union),
Shirika la Misaada la Uingereza (UK aid) na Shirika la Misaada la
Marekani (USAID).
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 MAONI YAKO:
Post a Comment