September 05, 2015

Saed KubeneaKatika taarifa yake kwa Mwanahalisi Online, Saed Kubenea, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL) wachapishaji gazeti la MwanaHALISI, (ambaye amechimba kwa undani sakata la Richmond lililotokea mwaka 2007) amesema: 

NIMEMSIKILIZA kwa makini, Dk. Willibrod Slaa, aliyekuacha Ukatibu mkuu wa Chadema na katibu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akizungumza katika mahojiano na kituo cha telebisheni cha Star TV.

Dk. Slaa ambaye ni msomi wa thiolojia, amemtuhumu Mgombea Urais anayewakilisha UKAWA, Edward Lowassa kwamba ni fisadi na hafai kuchaguliwa na wananchi.

Ikiwa ni mara yake ya pili kutokeza hadharani tangu aliposusa kufanya kazi za katibu mkuu katikati ya mwezi Julai mwaka huu, ameeleza kwanza Watanzania wamchague “Mgombea mwenye nafuu ya ufisadi...” akamtaja John Pombe Magufuli.

Kwa taarifa mpya aliyonayo na ambayo aliitumia katika mkutano wake na waandishi wa habari Jumanne iliyopita, kuhusu sakata la Richmond, aliipata kutoka kwa Dk. Harrison Mwakyembe, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati Teule ya Bunge, juu ya Richmond.

Kubenea amesema ameshindwa kuvumilia taarifa anazozitoa Dk. Slaa kuhusu sakata hilo na sasa ataeleza anachokijua kuhusu sakata la Richmond na msukumo uliopo hata Dk. Slaa kujitokeza wakati huu wa kampeni za uchaguzi katika mlengo wa kumshambulia na kumchafua Lowassa.

“Niliamua kutojibizana na Dk. Slaa – rafiki yangu wa miaka mingi – katika mradi wake huu. Lakini kwa hapa alipofika, uvumivu umenishinda. Sitaruhusu mtu mzima, anayejiita padri na ambaye alitaka kuwa rais wetu, kuendelea kulindanganya taifa na kuwapotosha wananchi.

“Hivyo basi, nimeamua kuanzia leo hii, kukabiliana na Dk. Slaa kwa kila kona ili ukweli ufahamike. Kwa kuanzia, leo hii – Jumamosi, naelekea mkoani Mbeya ambako nitahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara katika jimbo la Kyera, linaloshikiliwa na Mwakyembe, swahiba mpya wa Dk. Slaa.

“Nikiwa Mbeya nitaeleza ukweli wa kilichotokea na kile ambacho Dk. Slaa anakificha.

“Aidha, nikirejea Dar es Salaam, nimepanga kuitisha mkutano na waandishi wa habari, kueleza ukweli uliokamilika kuhusu Dk. Slaa na mkewe Josephine Mushumbuzi na sababu ya yeye kususia chama.”


Imenukuliwa kutoka MwanaHALISI Online

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE