March 11, 2015

 
 Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
 Siku chache baada ya kifo na maziko ya aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), Kapteni John Komba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amemlilia akieleza kuwa ni mtu ambaye alikuwa ‘muumini asiyeyumba wa safari ya matumaini.’
 
Marehemu Komba ambaye alizikwa Jumanne iliyopita kijijini kwake Lituhi, anatajwa kuwa alikuwa rafiki wa karibu na Lowassa.
Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, alisema moyo wake unabubujika machozi ya damu kwa kuwa marehemu Komba alimshawishi agombee urais na amefariki dunia kabla hajampa jibu la kukubali au kukataa.
 
Alisema Kapteni Komba alikuwa mmoja wa makamanda wa kuongoza harakati za kumshawishi ajitose kwenye kinyang'anyiro cha urais.
 
“Ulipaza sauti bila woga kuelezea imani yako kwangu. Kapteni naumia sana umeondoka bila ya kukupa jibu la kukubaliana na ushawishi wako au la...kwa hakika Chama kimepata pigo.”
 
“Hivi ni kweli sitasikia tena sauti yako Kapteni Komba! Mbona umeondoka bila ya kuniaga ndugu yangu! Moyo wangu unabubujika machozi ya damu," alisema Lowassa katika taarifa hiyo.
 
Alisema siku tatu kabla ya Komba kukutwa na umauti, alimtumia ujumbe kupitia kwa wasaidizi wake akimwambia ‘Mwambie Edward akija aje kuniona mimi sijisikii vizuri.’
 
“Maneno yako kwa mmoja wa wasaidizi wangu siku tatu kabla ya umauti kukupata, yanazunguka akilini mwangu...Kapteni Komba, mimi na wewe tumepigana vita nyingi kwa maslahi ya Chama na nchi yetu na tulishinda vita hivyo. Lakini bado tulikuwa tunaendelea na mapambano ya kumnasua Mtanzania katika umaskini,” alisema Lowassa.
 
Aliongeza: “Ni nani asiyejua mchango wako katika ushindi wa chama chetu katika ngazi zote. Nyimbo zako ndiyo adhana au kengele ya kuwakusanya waumini (wana-CCM na wananchi), katika mikutano ya Chama. Komba ulikuwa nembo ya chama chetu.”
 
Alisema Komba ameondoka, lakini ameacha alama katika ulimwengu wa siasa hususan katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Katika taarifa hiyo, Lowassa alisema kwa kuwa alishirikiana na Komba kwenye nyakati za matatizo na furaha, atashirikiana na Chama kuendeleza pale alipoachia kutatua matatizo ya familia. 
 
Kapteni Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu na mara kadhaa Ofisi ya Bunge ilimpeleka India kwa matibabu. Pia alikuwa na tatizo la kisukari ambalo ndilo lililochukua maisha yake.
 
Lowassa ametoa taarifa hiyo nzito akiwa ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kuwania nafasi ya urais.
 
Wengine wanaotajwa na ambao wameshajitangaza kujitosa kuwania nafasi hiyo ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na  Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
 
Wengine ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangwalla na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
 
Wamo pia Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.
 
WARAKA WENYEWE
Hivi ni kweli sitosikia tena sauti yako Captain Komba! Mbona umeondoka bila ya kuniaga ndugu yangu! Moyo wangu unabubujika machozi ya damu.
 
Maneno yako kwa mmoja wa wasaidizi wangu siku tatu kabla ya umauti kukupata  kwamba “mwambie Edward akija aje kuniona mimi sijisikii vizuri” yanazunguka akilini mwangu.
 
Captain Komba, mimi na wewe tumepigana vita nyingi kwa maslahi ya chama na nchi yetu… na tulishinda vita hivyo. Lakini bado tulikuwa tunaendelea na mapambano ya kumnasua Mtanzania katika umaskini.
 
Komba ulikuwa muumini usiyeyumba wa “Safari ya Matumaini”. Ulikuwa mmoja wa makamanda wa kuongoza harakati za kunishawishi niwanie urais kupitia chama chetu. Ulipaza sauti bila woga kuelezea imani yako kwangu. Captain, naumia sana umeondoka bila ya kukupa jibu la kukubaliana na ushawishi wako au la.
 
Kwa hakika chama kimepata pigo. Ni nani asiyejua mchango wako katika ushindi wa chama chetu katika ngazi zote. Nyimbo zako ndiyo adhana au kengele ya kuwakusanya waumini (wana CCM na wananchi) katika mikutano ya chama. Komba ulikuwa nembo ya chama chetu.
 
Komba umeondoka, lakini umeacha alama katika ulimwengu wa siasa hususan katika chama chetu. Daima nitakukumbuka ndugu yangu, naamini kabisa yale mapambano utayaendeleza huko ulikoenda ambako sote tutakuja.
 
Nakuahidi ndugu yangu, kama tulivyokuwa pamoja katika matatizo na furaha zetu, mimi na chama chetu tutaendeleza pale ulipoachia kutatua matatizo ya familia. Namuomba Mungu anipe nguvu na moyo wa kuyafanya hayo. Pumzika kwa amani rafiki yangu, ipo siku isiyo na jina tutaonana.

Related Posts:

0 MAONI YAKO:

Post a Comment

Popular Posts

WADAU

BLOG ZINGINE