Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ametoa rai kwa
wakazi wa jiji hili na wageni wanaoingia jijini humu kutoka katika mikoa
mbalimbali kupuuza taarifa za sauti zinazosambazwa kwenye mitandao ya
jamii kuwa polisi wanawakamata hovyo wanaolala mchana kwenye nyumba za
wageni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Kamanda Sirro leo, habari zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii
pamoja na zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti, kwamba polisi
wanawakamata watu hao kwa madai ya uzururaji na uzembe ni uvumi.
Kamanda Sirro alisema kwa nia ovu,
taarifa hizo zimedai kuwa hatua hiyo ni kutekeleza agizo la Rais John
Magufuli la ‘Hapa Kazi Tu’, jambo ambalo si la kweli.
“Ninawatoa hofu raia wema kuwa
tunaendeleza operesheni kuwasaka watuhumiwa wa makosa mbalimbali
wakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba za kulala wageni kinyume cha
sheria kwa kuendesha gesti bubu,” amesema.
Amesema katika taarifa yake hiyo kuwa
uchunguzi umebaini kuwepo na nyumba za kulala wageni zinazoendesha
biashara kiholela kwa kuhifadhi wahalifu, wakiwemo wanawake na wanaume
wanaouza miili yao (dada na kaka poa).
“Ni wajibu wa polisi kufanya ukaguzi mara kwa mara kwenye nyumba za wageni, hoteli
,
migahawa, vilabu vya vileo na kumbi za starehe zinazokesha,” alisema na
kuongeza kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Sirro amewataka wafanyabiashara wa
nyumba za kulala wageni kufuata taratibu za kupokea wageni kwa kuandika
majina yao kwenye vitabu, kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu
wanazotoka na watakapomtilia mashaka mteja yeyote watoe taarifa kwenye
kituo chochote cha Polisi.
Aliwataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa
na wajumbe wa Nyumba 10 wawajibike kuwatambua wageni wote wanaoingia
kwenye himaya zao na kuwachukulia hatua stahiki wanaobainika kuwa ni
wahalifu, ili kuimarisha usalama.
0 MAONI YAKO:
Post a Comment